Mtoto mmoja aliyefahamika kwa jina la Yumwema Charles (4), amefariki dunia na wengine 19 wamejeruhiwa baada ya kutokea ajali iliyohusisha basi la Happy Nation lililokuwa likitokea jijini Dar es Salaam kwenda mkoani Katavi.
Basi hilo lililigonga lori la Kampuni ya Dangote lililokuwa limeegeshwa kando mwa barabara katika kizuizi cha Kata ya Pangawe wilayani Sikonge, mkoani Tabora.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkaoni Tabora, Costantine Mbogandi, akizungumzia ajali hiyo leo Jumatano Julai 17, 2024, amesema chanzo chake ni uzembe wa dereva wa basi la Happy Nation ambaye hakuwa akifuata sheria za usalama barabarani.
"Ni kweli alfajiri ya leo maeneo ya Pangale, Wilaya ya Sikonge, ilitokea ajali iliyohusisha magari mawili; basi lenye namba za usajili T.519 DXH aina ya Higher, mali ya Kampuni ya Happy Nation, likiendeshwa na dereva Wilson Sinai, maarufu ‘Nyoma’ na lori lenye namba za usajili T.295 EBS mali ya Kampuni ya Dangote lililokuwa limepakia simenti," amesema Kamanda Mbogandi.
Amesema katika ajali hiyo, mtoto mmoja aliyefahamika kwa jina la Yumwema Charles (4) amefariki dunia na watu watatu wamepata majeraha makubwa.
Amewataja majeruhi ni pamoja na Michael Masanja (31), Maftaha Mapunda (38) na Nathan Makungi (48).
Amesema dereva wa basi hilo anashikiliwa na Polisi na dereva wa lori amekimbia kusikojulikana.